Matthew 28

Isa Afufuka

(Marko 16:1-10; Luka 24:1-12; Yohana 20:1-10)

1 aBaada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.

2 bGhafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaenda penye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. 3 cSura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.

5 dYule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Isa aliyesulubiwa. 6 eHayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. 7 fKisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ”

8Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, bali wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. 9 gGhafula, Isa akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. 10 hNdipo Isa akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”

Taarifa Ya Walinzi

11 iWakati wale wanawake walikuwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. 12Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kutunga hila, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha 13 jwakiwaambia, “Inawapasa mseme, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ 14 kKama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.” 15Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi mpaka leo.

Isa Awatuma Wanafunzi Wake

(Marko 16:14-18; Luka 24:36-49; Yohana 20:19-23; Matendo 1:6-8)

16 lBasi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Isa alikuwa amewaagiza. 17Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. 18 mIsa akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 nKwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 onanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
Copyright information for SwhKC